Naanza kwa kukuomba samahani
Kuandika kwa lugha hii legevu
Nilijaribu lakini sikuweza
Kuyasarifu maneno matamu
Kwa lugha muafaka ya kimapenzi
Mara nyingine ninaahidi
Kutakalamu kwa lugha inayofaa
Bidii nitafanya
Kuyaelewa machungu na matamu yanguKwa lugha tukufu isiyo yangu
Badala ya hiki kishairi duni,
Nitakwandikia poem
Nitajitahidi mpenzi
Maneno kuyaelewa
Si kwa jicho la kwangu kijijni
Bali kwa mboni na urazini wa kule kulikotukuka
Nitayatongoza machozi yangu
Kububujika kwa vokali na konsonanti za kimombo
Makali ya moyo wangu kulipuka kwa Kireno,
Kitaliani au Kituruki
Badala ya huu msamiati nilokujazia hapa,
Nitakuwa na vocabulary Mpenzi nitakusifu
Kwa majina ya mimea, wanyama na ndege
Wasiopatikana kwetuNitakutungia koja
Nilirembe kwa vito na maua ya nchi za baridi
Au mimea ya jangwaniNisamehe kwa sasa mpenzi
Naikumbuka tu lugha yangu
Ilonitoa tumboni mwa mama
Ninajua mpenzi
Ni vigumu kwangu kujieleza
Vigumu kwako kuelewa
Nyimbo za nyumbani kwetu kijijini
Ambako tulitembea pamoja tukivikwea vilima
Mikono yetu ikiwa kama sumaku na chuma
Ni vigumu mpenzi
Wewe kuzikumbuka zile harufu
Za mimea iliyotushangilia
Katika sherehe yetu ya mahaba na huba
Samahani mpenzi
Nimeianza barua hii kwa jina lako la kwanza
Wewe kwako ndilo jinalo la kati
Lililotumika kule nyumbani
Kabla ya kuujua mji,
Ugeni na ustaarabu wake.
Nitakuita kwa jina ajualo nyanyako kutamka
Nitajitahidi mpenzi
Kukujua kwa jina lako la mjini, dini na usasa wake
Niwie radhi mpenzi
Nitasema nawe kwa sauti
Wanaokuona na kukusikia laazizi
Wajue asili na usuli wako
Kwa muda wasikunasibishe
Na ungwana wa lugha uliyoizoea
Kwa mishangao waashame
Badala ya salaale
Wamake na kubweka ’gosh’!
Ningelipenda kuahidi kwenda nawe kupata mlo
Lakini natanguliza samahani
Ni haja yangu kukupeleka kula pizza
Lakini nimetafuta jinale katika lugha yangu
Nikakosa kabisa kabisa
Kwa hivyo mpenzi
Samahani zangu zikitangulia
Nakuahidi ugali wa wimbi
Samaki wa kuchemsha
Na mkunde wa kibakuli cha kando
Mpenzi hitari kula mtori
Jasiri pia kuonja makande,
Rojo la mrenda,
Mukimo na muthogoi.
Tutakula pia sageti,
anagu na wenzao.
Tutanyunyiza mafuta
Matamu ya samli,
Kisha tummemene tombo,
Alochomwa kwa makaa.
Jioni tutakaa
Chini ya uso wa mbalamwezi
Tukichoma ndizi,
Viazi na mihogo
Anga zitachanua
Kwa thureya ya nyota
Zikiimba wimbo bora
Wa mapenzi motomoto
Hewani kutafukizwa,
Uturi wa manukato
Ya samadi kavu inayoungua.
Samahani mahabubu,
Ingawa utatamani,
Kifukuza mbu muafaka,
Hii mwandani, haina viletamaradhi.
Sikio letu kichuna,
Tutamwazima bibi,
Babu akiwa mwenzake
Fikira zetu tuwape pia
Kutusafirisha mbali
Watupatie paukwa pakawa
Za miaka hii na iliyokuwa
Samahani mpenzi
Yameniishia maneno
Nimeyatesa macho yako,
Masikio na fikira zako
Misri kukurudisha
Japo kwa muda kidogo
Nikuandikiapo mara nyingine,
Nitakupeleka Zayuni
Kwenye miji mikuu ya utandawazi.
.....................................................
KALAMU ILIYOPOTEA
Ile iliyopotea, sasa nimeshaipata,
Kule likopotelea, nami nimeitafuta,
Kalamu ‘litokomea, kwa miezi hii sita,
Kalamu yangu, nishaishika.
Sasa naweleza nyote, mlionisubiria,
Kichofanya sinipate, kalamu ‘linikimbia,
Nikasaka kotekote, bado sikuifikia,
Kalamu yangu, nishaishika.
Leo nimeshaishika, nimeipata kalamu,
Kichobaki kuandika, yote ninayofahamu,
Kwandika pasi kuchoka, yote yote mumu humu,
Kalamu yangu, nishaishika.
Hamu mi sikuishiwa, daima nilitamani,
Tungo sikukaukiwa, zilibakia kichwani,
Imekuwa majaliwa, kalamu i kibindoni,
Kalamu yangu, nishaishika.
.................................
Majira hubadilika,
Miaka inasogea,
Nyasi nazo hunyauka,
Mimea kujiozea,
Lakini nina hakika,
Wewe hutonipotea.
Wewe unayo thamani,
Ya upendo ulo kweli,
U pekee duniani,
Ambaye wastahili,
Kukupa yalo moyoni,
Kwa pendo letu wawili.
Mi nawe twapendezana,
Kwa pendo lililoshiba,
Hakika tunatoshana,
Kwa dhati pia kwa huba,
Pendo tunalopeana,
Linayo tele mahaba.
Wanipa mie furaha,
U zawadi maishani,
Kuwa nawe kuna raha,
Ni raha iso kifani,
Nafurahi kwa madaha,
Waridi langu moyoni.
...........................
kitaka kunipenda nipende taratibu,
Ukizidisha utaniuwa mwenzio!
Ukitaka kunipa raha basi iwe taratibu,
Ukizidisha utaniuwa mwenzio!
Ukitaka kuniumiza niumize tu kidogo,
Ukizidisha utaniuwa mwenzio!
Ukitaka kunitesa sikuzuwii ila taratibu,
Ukizidisha utaniuwa mwenzio!
Moyo wangu, moyo wangu uendee taratibu,
Ukizidisha waniletea masahibu!
Usiku silali ukiniuliza we ndo sababu,
Taratibu basi utaniuwa mwenzio!
Moyo wangu, moyo wangu unauadhibu,
Basi fanya japo taratibu!
Niondolee madhila yaliyozidia hesabu,
Utaniuwa mwana wa mwenzio!
Taratibu, twende taratibu basi taratibu,
Nitese tu kidogo ukipata sababu!
Ukizidisha moyo wangu wauharibu,
Ukizidisha utaniuwa mwenzio!