Muhashamu muhashamu, ujumbe nakutumia,
Pokea zangu salamu, za mashamshamu pia,
Nimepatwa na wazimu, siachi kukuwazia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Kama mapenzi ni sumu, basi imeniingia,
Nakesha mang’amung’amu, wewe kukufikiria,
Yanienda kasi damu, moyo h’utaki tulia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Moyo ‘ngekuwa na zamu, nawe ningekupatia,
Uzionje zilo humu, zilivyojaa hisia,
Halisi zilizo tamu, wewe nizo kupatia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Naganda kama sanamu, wewe ninakungojea,
Zingali siku zatimu, moyo khali wasemea,
Kwa pendo hili adhimu, wewe tuu kukupea,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Wao wanonituhumu, hawawezi nisumbua,
Kukupenda ‘melazimu, vinginevyo naugua,
Ungali yangu naumu, hapa chini yake jua,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Penzi lisilo awamu, kusema litapungua,
Penzi daima dawamu, moyo wangu we chukua,
Kukupenda ni swaumu, pendo nal’ombea dua,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Sihesabu tarakimu, penzi linavyozidia,
Bali ni mastakimu, hakuna ‘nokufikia,
Hakuna wa kukaimu, nafasi ‘nokupatia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Uzuri wako adimu, wengi wanaulilia,
Wazikoleza fahamu, daima nakuwazia,
Kukupenda ni jukumu, mwingine sitomwachia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Kwako siishiwi hamu, kila siku wazidia,
Mapishi yako matamu, mtu sito’bakishia,
Hakika wewe mwalimu, cheti nakutunukia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.
Beti kumi zimetimu, wewe nimekwandikia,
Nitapiga hata simu, maneno nikakwambia,
Daima nitajihimu, wimbo nikakuimbia,
Mwenziyo sinayo khali, sijiwezi juu yako.