mmmmh


oo

Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

mapenzi si kamari

Mapenzi si kamari, ridhia kwa moyo! Ni sentesi ambayo kama mtu akitafakari kwa kina kuna kitu kitaingia kichwani mwake.

Kuna baadhi ya watu huwa wanabahatisha katika mapenzi, yaani mtu anakuwa na mpenzi hata kama ana uhakika kuwa hana mapenzi naye ya dhati, anafanya hivyo kwa kujilazimisha tu. Huo ni upuuzi usioweza kuneemeka.

Mapenzi ni ridhaa, yanatokea moyoni. Unajua moyo wako ndiyo wenye uwezo wa kufanya uchaguzi sahihi na si uchaguzi bali uamuzi wa moja kwa moja, maana moyo ndiyo wenye uwezo wa kupenda na kuhifadhi pendo ndani yake.

Wakati mwingine huwa najiuliza, kwanini mapenzi yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Lakini wakati wengine wakiumizwa, wapo ambao kwao mapenzi ni burudani. Unajua sababu ni nini rafiki yangu? Kanuni tu, baaasi!

Yaani ukifuata kanuni za mapenzi, ukaachana na tamaa na kuuachia moyo wako ufanye maamuzi wenyewe, utayafurahia maisha yako ya kimapenzi. Mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi.

Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.
Hapa mapenzi ya ulaghai hayahusiki, nazungumzia juu ya mapenzi ya dhati kutoka katikati ya moyo wa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Mapenzi hayo hukamilika baada ya wawili kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiye unayempenda, ujue kuwa unakuwa mtumwa wa mapenzi!

Kama ndivyo, kwanini uwe mtumwa? Msomaji wangu huna sababu ya kuingia katika uhusiano tata, ambao mwisho wa siku utaishia kulia huku mtu wa kukubembeleza akikosekana. Kipo kitu cha kujifunza hapa rafiki yangu, hebu twende tukaone.

MOYO WAKO UMEMPENDA?
Suala la mapenzi uhusisha moyo zaidi, moyo wako ndiyo mwamuzi wa mwisho katika hilo, hata siku moja usikubali kulazimisha moyo wako kwa mtu ambaye hujaridhia kuwa naye. Achana na imani kwamba ukimkataa kijana fulani basi bahati inaweza kukupita, nani amekudanganya?

Suala la kuolewa halina bahati, Mungu mwenyewe ndiye mpangaji wa hili, unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa?

Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi! Mapenzi ni nguzo katika maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na mwandani wako. Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe.

Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza nao, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwanini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu!

Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako utatetemeka juu yake na kutamani akuambie kitu fulani kwa kuwa anakuwa ameshauteka moyo wako ghafla.

Hii inaama kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana na lazima utamkaribisha moyoni mwako!

...SI KAMARI
Utakuta msichana anaingia katika uhusiano na mwanaume ambaye hana maopenzi naye ya dhati lakini kwa kuwa mwanaume huyo ana mali na uwezo wa fedha, huamua kumkubali kwa misingi ya kuwa na tamaa ya mali zake.

Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo.
Kwa maneno mengine, anajidanganya kwamba atacheza kamari ya mapenzi.

“Fedha anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitajitahidi kumpenda taratibu,” baadhi ya wasichana huwaza hivyo.

Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa.

Wataalamu wa mambo ya uhusiano huita ndoa hizo kuwa ni ‘Ndoa za Kichwa-kichwa’, usikubali kuingia katika ndoa ya aina hii hata siku moja! Mwishowe utajikuta ukilia kilio cha mbwa mdomo juu. Kaa ujue kwamba huwezi kucheza kamari ya mapenzi.

MADHARA YA KAMARI YA MAPENZI!
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutotosheka na mpenzi uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa mapenzi. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.

Hayo ndiyo mapenzi ya kweli bwana, siku zote utajisikia mwepesi na huru kwa mwenzako. Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea?

Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa, kuna siku lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo na kama ana hasira, anaweza kukua, kumuua aliyekufumania naye au kujiua yeye ili kukwepa fedheha. Hapo utauficha wapi uso wako? Fikiria kwa makini...

AMUA SASA
Kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kucheza kamari ya mapenzi, ni jambo gumu ambalo linaweza kuharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaweza kukusababishia ukajuta kuzaliwa.

Kuwa makini, maamuzi na yanayohusu mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana kwani unafanya hivyo huwa unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako ya baadaye.

Maisha yako ya kesho, huanza kwa mwanzo mzuri wa leo

visitors comments