Mapishi ya mboga mchanganyiko
Mahitaji
Viazi ulaya 4 vya wastani
Hoho jekundu 1/2
Hoho la njano 1/2
Hoho la kiajani 1/2
Njegere 1 kikombe cha chai
Carrot 1 kubwa
Broccoli kidogo
Cauliflower kidogo
Kitunguu 1
Nyanya 1/2 kopo
Swaum/tangawizi 1 kijiko cha chakula
Olive oil
Curry power 1 kijiko cha chakula
Coriander powder 1 kijiko cha chai
Tarmaric 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
1/4 ya limao
Matayarisho
Katika sufuria isiyoshika chini kaanga vitunguu mpaka viwe vya brown kisha tia swaum/tangawizi na spice zote kaanga kwa muda mfupi kisha tia nyanya na chumvi. pika mpaka nyanya ziive kisha tia vegetable zote na vimaji kidogo sana na kisha kamulia limao, baada ya hapo punguza moto na kisha funika na zipike mpaka vegetable zote ziive na rojo ibakie kidogo. Baada ya hapo mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa
••.••mαpishi ℓσαđiиg••.•.••
.............
MAPISHI YA CHOROKO
Mahitaji
Choroko kikombe 1 na nusu
Nazi kopo 1
Kitunguu kikubwa 1
Nyanya 1/2 kopo
Swaum 1 kijiko cha chai
Curry powder 1 kijiko cha chai
Chumvi kiasi
Olive oil
Pilipili nzima
Matayarisho
Loweka choroko usiku mzima kisha zichemshe mpaka ziive na ziweke pembeni. Baada ya hapo saga pamoja nyanya, kitunguu, na swaum kisha vipike mpaka maji yote, baada ya hapo tia mafuta na curry powder, pika mpaka nyanya zitoe mafuta kisha tia choroko,tui la nazi, maji nusu kikombe,pilipili na chumvi, kisha koroga vizuri na uache ichemke. Pika mpaka tui la nazi litakapoiva na rojo ibakie kidogo sana, kisha ipua na mboga yako itakuwa tayari kwa kuliwa. Mi huwa napenda kuila na wali ila hata na ugali au chapati inaenda pia.
••.••mαpishi ℓσαđiиg••.•.••
.............
MAPISHI YA KABICHI
Mahitaji
Kabichi 1/2 kilo
Nyanya ya kopo 1/2
Kitunguu 1
Curry powder 1/2 kijiko cha chai
Chumvi
Olive oil
Matayarisho
Kwanza kabisa bandua magada ya juu ya kabichi, kisha ioshe na uikaushe maji baaba ya hapo katakata kabichi (inapendeza zaidi kama ikikatwa nyembamba) kisha saga pamoja nyanya na kitunguu. Baada yahapo tia katika sufuria ya kupikia, ipike mpaka maji yote yatakapokauka kisha tia chumvi, curry powder na mafuta pika kwa muda kiasi kisha tia kabichi na upunguze moto. Pika mpaka kabishi itakapoiva kisha ipua na itakuwa tayari kwa kuliwa. Unaweza kuila kwa wali au ugali.
••.••mαpishi ℓσαđiиg••.•.••
.............
TAMBI ZA SAUSAGE NA CAROTTE
Tumezoea kupika tambi na nyama ya
kusaga au kuzichemsha zenyewe, leo nawaletea mapishi tofauti ya tambi.
Mahitaji
1. Tambi
2. Sausage
3. Karoti kubwa 1
4. Chumvi
5. Mafuta
Matayarisho
1. Bandika sufuria jikoni na maji kiasi na uweke chumvi kiasi.
2. Kata kata sausage zako vipande vidogo vidogo.
3. Kwangua karoti kisha katakata vipande vidogo vidogo vya nusu duara.
4. Maji yakichemka weka mafuta kisha weka tambi na funikia zichemke.
5. Zikianza kuiva weka sausage na karoti, acha viive pamoja.
6. Epua, chuja maji na andaa mezani tayari kwa kuliwa.
••.••mαpishi ℓσαđiиg••.•.••
WALI WA BIRIANI
Mchele kilo 1
Nyama kilo 1
Samli ½ kilo
Mbatata ½ kilo
Vitunguu maji kilo 1
Thomu gram 150
Tangawizi mbichi gram 150
Hiliki gram 50
Mdalasini gram 100
Mtindi painti 1
Siki kiasi
Majani ya nanaa fungu moja
Chumvi kiasi
Zaafarani kidogo (irowekwe kwa maji ya moto nusu kikombe cha kahawa)
Tungule ilosagwa
Tungule ya kopo
1 Menya vitunguu maji uvioshe uvikate. teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange bila ya kuvivuruga mpaka viwe vyekundu. Vichuje uvitoe halafu vitandaze katika sinia.
2 Twanga mdalasini na hiliki mpaka viwe laini kama unga. Menya thomu uitwange pamoja na tangawizi mbichi.
3 Kata nyama vipande vikubwa kisha tia chumvi na vitu ulivyovisaga (yaani tangawizi mbichi na thomu) vile vile tia unga unga wa mdalasini na hiliki pamoja na mtindi wa maji. Pika mpaka karibu nyama kuiva kabisa ndipo utie mbatata. Ukiona mbatata zimeshaiva tia siki.Usiache kukauka kabisa, bakiza rojorojo. Tia maji katika sufuria na chumvi yakichemka tia mchele. Acha utokote, angalia kiini cha wali ukiona umeshaiva uchuje.
4 Angalia sufuria ya nyama na rojo lake lisiwe limekauka kabisa, lazima ziwe na maji kidogo. Chukua vile vitunguu ulivyovikaanga vikapoa uvinyunyuzie juu ya masalo yote (usikoroge). Halafu utie mchele uliouchuja, nyunyuzia maji ya zaafarani juu ya wali wote halafu unyunyuzie samli ile uliyochuja kutoka kwenye vitunguu ulivyovikaanga ienee juu ya wali wote. Kisha funika upalie makaa.
5 Wali ukishakuwa tayari utaupakua. lakini unapotaka kuupakua lazima kwanza uutoe wali wote mweupe uutie katika chombo chengine, halafu uyakoroge masalo yachanganyike sawasawa kisha ndio uyatie juu ya wali katika kila sahani.
.....................
WALI WA PILAU
Mchele kilo 1
Nyama kilo 1
Samli ¼ kilo
Vitunguu maji ½ kilo
Vitunguu thomu gram 100
Tangawizi mbichi gram 100
Mdalasini gram 50
Hiliki gram 25
Pilipili manga gram 100
Zabibu gram 100
Chumvi kiasi
1 Teleka nyama utie chumvi na maji uipike mpaka iive. Baadae epua uiweke (ubakishe supu itakayotosha kuweza kuivisha mchele).
2 Menya vitunguu uvikate. Menya vitunguu thomu na tangawizi mbichi utwange pamoja. Menya hiliki uitwange pamoja na bizari nzima. osha vijiti vya mdalasini pamoja na chembe za pilipilimanga uziweke. Osha zabibu uziweke. Menya mbatata uzioshe uziweke.
3 Teleka sufuria tia samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Tia thomu na tangawizi mbichi uliyoisaga tia vipande vyote vya nyama bila supu, tia mbatata na viungo vyote ulivyovisaga na kuviosha, isipokuwa zabibu. Kaanga kwa muda mfupi, baadae tia supu yote. Ikianza kuchemka tia mchele, onja chumvi. Angalia kiini cha mchele, ukiona wali umeiva na kukauka, fukua kati utie zabibu zote na baadae funika upalie moto.
....................
WALI WA CHOOKO
Mchele kilo1
Chooko ½ kilo
Samli kiasi
Nazi 2 nzuri
Vitunguu thomu kiasi
Bizari nzima kiasi
Vitunguu maji kiasi
Hiliki kiasi
Mdalasini kiasi
Chumvi kiasi
Karafuu chembe 2 au 3
1 Osha mchele pamoja na chooko uweke pembeni.
2 Kuna nazi uchuje tui kama la wali wa nazi uliweke.
3 Menya vitunguu maji, uvioshe uvikate uviweke. Menya vitunguu thomu uvitwange pamoja na bizari na hiliki. Osha vijti vya mdalasini na chembe za karafuu uziweke.
4 Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Baadae tia viungo vyote ulivyovitwanga utie na chembe za karafuu pamoja na vijiti vya mdalasini. Kisha tia tui la nazi. Likianza kufumba tia mchele pamoja na chooko zake utie na chumvi. Acha utokote mpaka wali ukauke. Ukishakauka funika upalie moto.
....................
PILAU YA KUKU
Mchele kilo 1
Kuku mkubwa 1
Samli ¼ kilo
Vitunguu ½ kilo
Thomu gram 100
Tangawizi mbichi gram 100
Mdalasini gram 50
Hiliki gram 50
Bizari nzima gram 25
Zabibu gram 100
Pilipili manga kiasi
Chumvi kiasi
1 Mkate kuku umpike kwa maji na chumvi mpaka aive. wakati wa kumuepua angalia kuwa ana supu itakayotosha kuivisha mchele.
2 Menya vitunguu uvioshe na kuvikata pamoja. Menya thomu na tangawizi mbichi pamoja. Twanga bizari nzima na hiliki. Osha vijiti vya mdalasini na chembe za pilipili manga uweke kando.
3 Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia thomu na tangawizi mbichi pamoja na viungo vyote vilivyobakia. Kaanga kidogo kisha tia mbatata na vipande vya kuku na umimine supu yote. Ikianza kuchemka tia mchele. Acha utokote. Onja chumvi.Angalia, ukiona wali umeshakauka fukua kati utie zabibu kisha palia moto.Wali ukishakauka utaupakua. kama unavyopakua wali wa pilau na nyama.
.......................
BOKOBOKO
Ngano nzima kilo 1
Nyama kilo 2
Mchele ¼ kilo
Samli ½ kilo
Vitunguu kiasi
Thomu kiasi
Bizari nzima kiasi
Hiliki kiasi
Mdalasini kiasi
Giligilani kiasi
1 Teleka ngano na nyama na maji upika mpaka viive viwe laini sana. Osha mchele utie. Saga vitunguu pamoja na viungo vyote uvitie na uendelee kuvipika vyote pamoja huku unavikoroga mpaka vichanganyike na viive vyote na maji yote yakauke. (Unaweza kutia chumvi kidogo ukipenda). Funika upalie moto.
2 Utakapokauka funua uanze kulisonga bokoboko. Lisonge mpaka lishikane sawasawa halafu liipue.
3 Chukua samli uichemshe pamoja na hiliki kisha kila unapopakua utakuwa unalilazalaza na kulitengeneza kwa samli. Wengine hupenda kutengeneza kishimo kati kati yake na kukijaza samli ya moto. Watu wengine hupenda kulila tupu, na wengine hula kwa sukari au kwa mchuzi wake ambapo hutengenezwa mahsusi.
.........................
TAMBI ZA NAZI
Tambi kilo 1
Sukari ¼ kilo
Nazi kavu 2
Hiliki kiasi
Arki kiasi
1 Teleka maji, yakichemka zitie tambi zichemke kidogo, kisha zimimine katikachujio au kumto yatoke maji yote.
2 Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki utwange utie katika tui.
3Liteleke tui ulipike na huku unalikoroga, kisha tia tambi utie na sukari uwe unazigeuzageuza kwa mwiko mpaka tui lote likauke lianze kutoa mafuta.
4 Ziepue uache zipoe. baadae zipakue.
....................
TAMBI ZA KUKAANGA
Tambi kilo 1
Sukari ¼ kilo
Samli ¼ kilo
Hiliki kiasi
Arki kiasi
Zabibu (zioshe uziroweke kidogo kwenye maji ya moto).
1 Zichukue tambi uzivunjevunje katika sinia au ungo.
2 Teleka sufuria juu ya moto utie samli. Ikichemka tia tambi zote uwe unazikaanga mpaka zipige wekundu. Tia sukari, hiliki au arki pamoja na maji ya moto. Acha zichemke mpaka uone kiini cha tambi kisiwe laini sana na maji yote yakauke.
3 Ziepue uache zipoe kidogo. Baadae zimimine kwenye sahani. chukua zabibu upambie juu yake.
....................
SAMAKI WA MAYAI
Samaki (nguru) kilo1
Vitunguu kilo 1
Tungule kilo 1
Samli ½ kilo
Mayai 6
Thomu kiasi
Pilipili manga kiasi
Bizari nzima kiasi
Ndimu kiasi
Chumvi kiasi
1 Mkatekate samaki umtie chumvi, pilipili na ndimu umkaange kisha mtoe umuweke.
2 Kata vitunguu, saga tungule, thomu na viungo vyote vilivyobakia.
3 Teleka sufuria utie samli. Ikichemka tia vitunguu uvikaange mpaka vipige wekundu. Tia tungule, thomu pampja na viungo vyote. CHUKUA VIPANDE Vyote vya samaki uvitie, kisha tia ndimu na maji kidogo. Kisha onja, ukiona kila kitu sawa vunja mayai moja baada ya jengine uwe unayaweka juu ya samaki kwa mpango mzuri bila ya kuharibu viini vyake.Funika kwa mkungu upalie moto mdogo mdogo juu yake ili mayai yapate kuiva.
4 Angalia, ukiona epua upakue kwa upole bila ya kuharibu mpango wa mayai
....................
SAMAKI WA ROJO
Samaki mkubwa 1
Vitunguu kilo 1
Tungule kilo 1
Samli ½ kilo
Pilipili manga kiasi
Thomu kiasi
Ndimu au ukwaju kiasi
Bizari nzima kiasi
Chumvi kiasi
1 Mwoshe samaki (usimkate) umtie pilipili, chumvi na ndimu.
2 Kata vitunguu, saga thomu, tungule pamoja na viungo vyote vilivyobakia.
3 Teleka chuma utie samli. ikichemka mtie samaki umkaange vizuri mpaka aive. Mtoe umtie katika kombe au sahani kubwa ya shimo.
4 Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia viunguu uvikaange mpaka vipige wekundu. Tia tungule na viungo vyote. Tia chumvi, ndimu na maji kidogo. Wacha ichemke mpaka ikauke. Chukua rojo lote umimine juu ya samaki lakini kwa utaratibu, umfunike samaki wote kwa rojo.
......................
SAMAKI WA KUKAUSHA
Samaki kilo 1
Vitunguu ½ kilo
Tungule ½ kilo
Nazi 2
Pilipili mbichi chembe 4
Ndimu kiasi
Chumvi kiasi
1 Mkate samaki vipande vipande umsagie chumvi na pilipili na umkamulie ndimu. Menya vitunguu uvikate, katakata tungule ukaushe vyote pamoja na samaki mpaka akaukie.
2 Kuna nazi uchuje tui zito utie juu yake upike mpaka likauke kabisa wala usikoroge. Akishakauka epua umpakue vizuri bila ya kumvuruga.
....................